Monday, 25 January 2016

Sisitizo la hatua za umoja dhidi ya njama za kuibua mifarakano nchini Iraq  Katika mwendelezo wa hatua za umoja wa wananchi wa Iraq, Waislamu wa Shia na Suni wa mji wa al-Miqdadiyah, katika jimbo la Diyala, hivi karibuni walisali Swala moja ya Ijumaa kwa pamoja Zaid al-Azawi, gavana wa mji wa al-Miqdadiyah amethibitisha habari hiyo na kuongeza kuwa, Waislamu hao wa Kisuni na Kishia walisali Swala ya pamoja katika Msikiti wa Laa Ilaha Illallaah uliopo katika mji mdogo wa Ashur. Azawi amesisitiza kuwa, katika swala hiyo ya umoja walishiriki pia maulama wa Kisuni na Kishia, wasomi na shakhsia wa makabila kadhaa ya mji huo. Ameongeza kuwa, Swala hiyo ilisaliwa kwa lengo la kudumisha umoja wa kidini na kitaifa katika kukabiliana na mirengo inayozusha tofauti, na kadhalika kuimarisha umoja wa wakazi wa al-Miqdadiyah wenyewe katika kukabiliana na changamoto ambazo zililikumba eneo hilo siku chache zilizopita. Kamanda wa polisi wa jimbo la Diyala, Jasim al-Sa'adi, amesisitiza kuwa, kusaliwa Swala hiyo ya umoja, kunaonesha umoja na ushirikiano wa wakazi wa eneo hilo katika kupambana na njama za kutaka kuibua tofauti na fitina baina yao. Naye Ra'ad al-Mas, mwakilishi wa jimbo la Diyala serikalini amesema kuwa, hivi sasa jimbo hilo hususan mji wa al-Miqdadiyah, lina usalama na amani . Inafaa kuashiria hapa kwamba, wiki iliyopita, mji wa al-Miqdadiyah, ulishuhudia mashambulizi ya kigaidi. Wakati huo huo mwakilishi wa Ayatullah Sistani, marjaa wa kidini nchini Iraq amewataka viongozi wa kisiasa na pande tofauti za nchi hiyo kuweka kando tofauti zao ili kukomesha mpasuko wa ndani nchini humo. Ahmad al-Swafi, amesema kuwa, hii leo Iraq inakabiliwa na matatizo na changamoto kubwa, zaidi likiwa ni jinamizi la kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh. Sanjari na kuwataka wanasiasa wa Iraq kufanya juhudi za kuimarisha usalama na amani nchini, amewataka wanasiasa kuyaunganisha makundi tofauti ya wananchi nchini humo. Hivi karibuni pia akiwa katika kikao cha baraza la mawaziri wa nchi hiyo, Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi akiyaonya makundi ya kisiasa juu ya njama za kuibua tofauti na kuvitaka vyama na makundi ya kisiasa nchini humo kufanya juhudi za kuhimiza umoja na mshikamano dhidi ya njama hizo za uhalifu ambazo zinawakabili Wairaq wote. Al-Abadi alivitaka vyombo vya habari kuimarisha umoja wa kitaifa na utulivu wa ndani ya nchi na kwamba wote kwa pamoja wanatakiwa kukabiliana na waharibifu wa mali za umma bila kujali tofauti. Akizungumzia njama za kuibua fitina za kikaumu na kimadhehebu nchini, Waziri Mkuu wa Iraq alisema kuwa, kufuatia kushindwa mtawalia magaidi wa kitakfiri wameelekeza nguvu zao kwenye suala la kuzusha fitina za kikaumu nchini humo na kwamba Wairaq wote wanatakiwa kuwa macho mbele ya njama hizo. 

No comments:

Post a Comment