Tuesday, 2 February 2016

Serikali yaipongeza Africa Muslim Agency


Yawashukuru wafadhili toka nchi za Kiarabu
Aboud Jumbe ataka amana itunzwe
Na Mwandishi Wetu, Moshi
Serikali imesema kwamba inathamini sana huduma za elimu, afya na ustawi wa jamii zinazotolewa na mashirika ya kidini. 
Aidha Serikali imetoa shukurani kwa wahisani wa miradi hiyo na kusisitiza kwamba Serikali inathamini sana juhudi za mashirika ya dini kwa mchango wake katika kuboresha huduma za jamii na kutoa misaada ya kibinaadamu. 
Hayo yapo katika salamu za Serikali za hivi karibuni katika hafla rasmi ya ufunguzi wa ‘Markaz Al Hudaa’ mjini Moshi ambayo ni taasisi rasmi ya huduma za Elimu, afya na 
ustawi wa jamii. Taasisi hiyo inamilikiwa na Shirika lenye Makao yake makuu Kuwait. 
Akiwasilisha salamu hizo za Serikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Prof. Philemon Sarungi; Afrisa Elimu Bw. Majili aliwataka wasimamizi wa Taasisi hiyo wafikishe salamu na shukrani za dhati za Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa ujumla kwa Shirika la Africa Muslim Agency na kwa wahisani wote wanaochangia huduma hizo. 
Kituo hicho cha Al-Hudaa kipo kata ya Kaloleni katika manispaa ya Moshi na kinajumuisha Al-hudaa Secondary School, Al-hudaa Daru-aytama; Eh-Ahsa Health Centre na Darul-Muuminat Vocatinal Centre. 
Taasisi zote hizo zishaanza kufanya kazi ambapo nyumba ya yatima inalea watoto 72, wakati Chuo cha ufundi kimesajili wanawake 25 ambao hujifunza ushonaji, misingi ya uhasibu, hisabati. lugha ya kiingereza na Maarifa ya Uislamu. Shule ya Sekondari itakuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita. 
Mzee Aboud Jumbe, Rais Mstaafu wa Zanzibar ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika sherehe hizo aliwaomba watakaonufaika na huduma hizo wazienzi na kwamba hiyo ni amana toka kwa Mola wao. 
Miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe hizo ni Sheikh Muhammad Al-Khamis toka Kuwait; Sheikh Twariq Al-Muhsin na Mar’wa Algamzi kutoka Emarati. 
Wao ni miongoni mwa Waislamu ambao swadaka zao husaidia kuendesha huduma hizo. Akielezea msimamo wa Shirika lake, Mkurugenzi wa Africa Muslim Agency Ofisi ya Dammam Sheikh Muhammad Al-Khamis alisema kuwa Waislamu wenye azma ya kutumia kile walichoruzukiwa kwa njia ya Allah wameamua kutoa huduma mbalimbali ili Waislamu na jamii kwa ujumla ifaidike kwazo. 
Africa Muslim Agency ina Ofisi kuu mjini Dar es Salaam ikiongozwa na Sheikh Shakir; wakati ile ya Kanda ya Kaskazini (Moshi) inaongozwa na Sheikh Majid.

No comments:

Post a Comment