Tuesday, 22 December 2015
Matangazo Yaliyopita
Jumanne, 22 Disemba 2015 19:22
Wabunge na Maseneta wa Burundi wapinga kutumwa wasimamizi wa amani wa AU

Bunge la Burundi limepinga mpango wa Umoja wa Afrika wa kutaka kutuma kikosi cha kusimamia amani katika nchi hiyo inayokabiliwa na mgogoro wa kisiasa.
Pascal Nyabenda Spika wa Bunge la Burundi sanjari na kuashiria kwamba, hakujatokea mauaji ya kimbari katika nchi hiyo amebainisha kuwa, hakuna udharura wa kutumwa kikosi cha Umoja wa Afrika nchini humo. Kwa upande wake Reverien Ndikuriyo, Spika wa Baraza la Seneti la Burundi amesisitiza juu ya tofauti baina ya mauaji na mauaji ya kimbari. Wabunge na wawakilishi wa Baraza la Seneti ambao walikutana siku ya Jumatatu katika kikao kilichowakutanisha pamoja wameitaka serikali ifanye kila iwezalo kukomesha mauaji yanayoshuhudiwa nchini humo ili izuie njama zinazofanywa za kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Ijumaa iliyopita Baraza la Usalama na Amani la Umoja wa Afrika llilipitisha uamuzi wa kutumwa kikosi cha askari elfu tano nchini Burundi na likaipatia serikali ya Bujumbura muda wa siku saba kuamua kama imeafikiana na uamuzi huo. Kabla ya hatua hiyo ya Bunge na Baraza la Seneti, msemaj wa ofisi ya Rais alikuwa ametoa radiamali yake kuhusiana na uamuzi wa Umoja wa Afrika wa kutaka kutuma kikosi cha kusimamia amani Burundi na na kutangaza kuwa, endapo AU itatuma kikosi hicho na kupuuza upinzani wa serikali kwa hatua hiyo, vikosi hivyo vitahesabiwa kuwa ni majeshi vamizi.
Hata kama wimbi la mauaji nchini Burundi linashuhudiwa kwa miezi kadhaa sasa, lakini mashambulio ya hivi karibuni ya wapinzani dhidi ya vituo vitatu vya kijeshi ambayo yalipelekea kutokea mapigano na watu 90 kuuawa, ni tukio ambalo liliitumbukiza nchi hiyo katika hatua nyingine mpya. Katika hali ambayo viongozi wa serikali wanadai kuwa, vitendo vyovyote vya utumiaji mabavu vya vikosi vya usalama vinafanyika katika fremu ya kurejesha amani na usalama, wapinzani wanasema kuwa, hatua hizo ni za ulipizaji kisasi dhidi yao na lengo lake ni kuwauwa wapinzani wa serikali.
Katika hali ambayo, weledi wengi wa masuala ya kisiasa wanatahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea vita vya ndani na kuanza mauaji mengine ya kimbari nchini Burundi, Umoja wa Afrika umetangaza kuwa hautaruhusu kuanza tena vita na kutokea mauaji mengine ya kimbari barani humo. Huku mgogoro wa Burundi ukishadidi kuna taarifa kwamba, duru nyingine ya mazungumzo ya amani inatarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini humo. Crispus Kiyonga Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye nchi yake ni mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mgogoro wa Burundi alitangaza hivi karibuni kwamba, njia bora kabisa katika mazingira ya hivi sasa ambapo hali ya usalama inazidi kudorora nchini humo ni kuanza tena mazungumzo kwa minajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo. Kiyonga amesema, viongozi wa kikaumu wana mambo kumi ambayo wanataka yatiwe katika ajenda ya mazungumzo ya tarehe 28 Desemba. Miongoni mwa mambo hayo ni duru ya tatu ya uongozi wa Rais Pierre Nkurunziza, jedwali la uchaguzi, hali ya usalama pamoja na serikali ya umoja wa kitaifa. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, zaidi ya watu 240 wameuawa huku wengine zaidi ya laki 2 wakilazimika kuyakimbia makazi yao, kutokana na kushadidi wimbi la mchafukoge nchini Burundi,tangu Aprili mwaka huu, baada ya chama tawala CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo. Wapinzani nchini Burundi wanasema kuwa, hatua ya Nkurunziza ya kugombea kiti cha Urais katika uchaguzi uliopita ilikuwa kinyume na katiba pamoja na mkataba wa amani wa Arusha Tanzania. Hapana shaka kuwa, ili kuiepusha Burundi isitumbukie katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka na za maana za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment