
Katika kile kinachoonekana ni kuvurugika mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa kisiasa visiwani Zanzibar, pande husika katika mazungumzo hayo zimetoa misimamo inayokinzana kikamilifu.
Dkt Ali Mohamed Shein wa Chama cha Mapinduzi CCM amewataka wafuasi wa chama hicho kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio, baada ya Maalim Seif Sharif Hamad wa Chama cha Wananchi CUF kuitisha mkutano wa waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kusema chama chake hakipo tayari kuona uchaguzi unarudiwa. Akihutubia mkutano maalumu wa CCM wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar uliofanyika katika Viwanja vya Maisara, Dkt Shein amewataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio pindi Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC itakapotangaza tarehe. Kwa upande wake Chama cha Wananchi CUF kimelaumu njama zinazofanywa na baadhi ya watu za kutaka kusababisha machafuko visiwani Zanzibar kwa kushikilia kurudiwa uchaguzi visiwani humo. Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea wa urais wa tiketi ya CUF katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015, amesema kuwa, hakuna mashiko yoyote ya kisheria yanayoweza kuhalalisha hatua ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ya kutangaza kufutwa uchaguzi huo na kusema kuwa, uchaguzi wa Oktoba 25 ni halali. Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliingia katika mgogoro wa kisiasa miezi miwili iliyopita baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura. Hatua hiyo ilichukuliwa katika hali ambayo matokeo yote ya uchaguzi wa majimbo 54 ya Baraza la Wawakilishi yalikuwa yameshatangazwa pamoja na karibu theluthi mbili ya kura za Urais
No comments:
Post a Comment